Mkuu wa Jeshi la polisi Wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Gilles Muroto amewataka wakazi wa Kata ya Sokoni One kila mmoja ajitahidi kufahamiana na jirani yake ili waweze kusaidana pindi uhalifu unapotokea katika eneo lao.
Hayo aliyasema juzi katika mkutano kati ya Jeshi la polisi, viongozi wa kata hiyo na askari wa vikundi vya ulinzi shirikishi ambao ulifanyika katika shule ya Msingi Sokoni One iliyopo Jijini hapa.
Muroto alisema kwamba, kuishi katika nyumba yenye “geti” kubwa ambayo inakuwa na mlinzi pamoja na mbwa si sababu ya kutovamiwa na wahalifu kwani wapo wengi ambao wanaishi maisha kama hayo lakini wanavamiwa na wezi au majambazi.
Alisema si vizuri kwa majirani kuishi kwa kujitenga kwani jirani ndio mtu wa kwanza kukupa msaada pindi uvamizi unapotokea ikizingatiwa kwamba maeneo mengi yana matatizo ya miundo mbinu kama vile ufinyu wa barabara ya magari hivyo ni vigumu kwa askari wa Jeshi la polisi kuyafikia kwa uharaka.
Katika kuboresha utendaji kazi wa vikundi hivyo, alisema kwamba ni vyema askari hao wakawa na sare maalum badala ya kufanya doria wakiwa wamevaa kiraia hali ambayo ni hatari kwao na pia inawatia wasiwasi hata wanaohojiwa.
Mbali na hilo pia aliwaahidi askari hao kuwapa vitambulisho vitakavyokuwa na saini yake pamoja na namba yake ya simu hali ambayo itasaidia kuwajengea imani wale watakaokuwa wanakutana nao hasa katika mahojiano.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi Mary Lugola aliwataka wananchi watoe ushirikiano kwa vikundi hivyo vya ulinzi shirikishi pamoja na Jeshi la Polisi katika kutoa kutoa taarifa zinazohusu uhalifu na wahalifu wenyewe.
Alimalizia kuwaelimisha askari hao kwa kuwaahidi kuwatembelea mara kwa mara katika eneo hilo na maeneo mengine ili mafunzo hayo yasambae kwa kila mwananchi hali ambayo itasaidia kujenga ushiriano mkubwa baina ya wananchi, Jeshi la polisi na vikundi vya ulinzi shirikishi.
Mpango wa uundaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi ulianzishwa Mwaka 2006 na Jeshi la Polisi nchini, ambao kwa kiasi kikubwa unasaidia kuwashirikisha moja kwa moja wananchi kushiriki katika suala nzima la ulinzi wa wao wenyewe pamoja na mali zao badala ya kuliachia Jeshi hilo pekee.
No comments:
Post a Comment