Saturday, 10 November 2012

Hamashauri ya wilaya Geita yapoteza milioni 60 kwa kufunga minada ya mifugo



 Mutta Symphorian na Meshaki Mpanda -Geita

Halmashauri ya wilaya ya Geita imepoteza mapato ya shilingi milioni 60  kuanzia kipindi cha   Julai hadi Oktoba mwaka huu, kutokana na karantini ya ugonjwa wa midomo na mapafu ulioathiri mifugo na kusababisha minada yote kufungwa.

Hilo limebainika katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani kilichofanyika wiki iliyopita katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya  hiyo, na kuhudhuriwa na Madiwani wa wilaya ya Geita na wilaya mpya ya Nyang'hwale.

Aidha sakata la kufungwa minada yote kumetokana na migogoro ya tozo ya chanjo kati ya Madiwani wa Wilaya hizo mbili  na idara ya  mifugo.

Wakizungumza kwa jazba madiwani hao wamesema kuwa kipindi cha  Februari mwaka huu mtaalamu huyo alitoza shilingi 300  kuchanja mnyama mmoja anayefugwa, Julai mwaka huu huu tozo hiyo ilipanda hadi shilingi 1000  kwa mnyama mmoja anayefugwa ili kukinga ugonjwa huo ampapo Agosti  mwaka huu  madiwani waliikataa tozo hiyo.

Madiwani hao walifafanua kuwa katika tozo hiyo mtaalamu huyo wa mifugo hakufuata utaratibu wa kukusanya mapato kwa kutotumia vitabu vya stakabadhi vinavyotambuliwa na Idara ya fedha.

Idara ya mifugo katika halmashauri hiyo ilifunga  minada yote ya mifugo maarufu ya Kasamwa,Katoro,Karumwa na Kamena kwa muda usiojulikana,

Ili kuondoa karantini hiyo idara ya mifugo imeomba kuchanja mifugo hiyo kwa shilingi 2500 kwa kila mnyama anayefugwa, lakini madiwani wametia msimamo wa kukataa tozo hiyo na kuapa kutomwona mtaalamu huyo akichanja mifugo katika Kata zao na kuagiza aondoke kwenye ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

"Hatumtaki daktari huyo wa mifugo katika Halmashauri ya wilaya hii, labda awe daktari wa mifugo wa ofisini" alifafanua Diwani  wa Kata ya Nzela Bw.Joseph Musukuma.

Uchunguzi uliofanyika na waandishi wa habari hizi unaonyesha kuwa tozo za chanjo katika wilaya za Chato na Bukombe mkoa wa Geita ni shilingi 500  kwa kila mnyama anayefugwa na hakuna karantini iliyowekwa kuhusu ugonjwa wa midomo na mapafu hadi sasa.

Diwani wa kata ya Nzela Bw. Joseph    Musukuma alisema  kuwa idara ya mifugo imekopa dawa za chanjo ya ugonjwa huo kutoka Mwanza zenye thamani ya shilingi milioni 70  ambazo idara hiyo ingezirudisha kwa tozo mpya ya shilingi 2500 kwa kila mnyama anayefugwa.

Naye mwenyekiti wa Tume  ya Madiwani kufuatilia sakata hilo alikiambia kikao cha Madiwani kuwa daktari wa mifugo Kanda ya Ziwa alimwambia Mwenyekiti huyo wa Tume kuwa ugonjwa huo hauui mifugo na kuongeza kuwa idara ya mifugo halmashauri ya  wilaya ya Geita imetumia nguvu kubwa kufunga minada hiyo.

Madiwani wameiomba serkali mkoani Geita kutumia daktari wa mifugo wa  wilaya jirani ili aje aondoshe karantini hiyo wilayani Geita na Nyan'gwale ili minada hiyo ifunguliwe haraka.

 Mkurugenzi wa halmashauri ya  Wilaya ya Geita Bw,Ali Kidwaka katika kikao hicho cha Madiwani alisema kuwa ana miezi michache tangu ahamie wilayani hapa, hivyo anahitaji muda ili azifanyie kazi tuhuma hizo na kutoa majibu katika kikao kijacho cha Madiwani.

No comments:

Post a Comment